Masau Bwire Awapa Neno Simba Sc

 Ameandika Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire


"Nawashukuru, nawapongeza sana wachezaji, benchi la ufundi, viongozi, wapenzi, wadau, mashabiki wa Ruvu Shooting FC na Simba SC, kadharika Watanzania wote Wazalendo, kwa kufanya vyema katika michezo yao iliyochezwa Februari 20, 2022, timu zote zikiwa ugenini.


Ruvu Shooting ikicheza na Tanzania Prisons, ligi ya NBC, uwanja wa Sokoine, Mbeya, ikashinda goli 0-1 dhidi ya Tanzania Prisons, imetoka nafasi ya 15 ya msimamo hadi ya 12.


Simba SC, wakicheza hatua ya makundi, kombe la Shirikisho Afrika na timu ya USGN huko Niger, iliwalazimisha wenyeji hao sare ya goli 1-1, matokeo ambayo yameifanya iongoze kundi kwa pointi 4.


Watanzania wazalendo, tuendelee kuiombea Simba SC, iendelee kufanya vizuri katika michezo ijayo ya mashindano hayo ya Shirikisho Afrika, ili izidi kuitangaza nchi kiuchumi, lakini pia zaidi sana katika ubora wa soka.


Wengi walidhani Ruvu Shooting ni timu dhaifu ilipofungwa na Simba SC magoli 7-0, bila kujua ilikuwa ikipitia machungu gani, wakajua ni ya kufungwa tu na yeyote, kumbe, masikini, wakasahau kuwa ni timu bora katika timu bora Tanzania, wawaulize Tanzania Prisons!


Simba SC ushindi wa bao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, walikosa tu huruma, walishindwa kujua wanacheza na wafiwa, wasio na ari ya kucheza, bila kujali, wakaja kwa nguvu zote, wakacheza kama kwamba wanacheza na Barcelona kweli, Mungu tu awasamehe, wametusababishia matatizo makubwa kwa jamii!


Matokea hayo ya 7-0 yalituathiri pakubwa, njiani tukipita, tunazomewa, tunaitwa eti wazee wa 7-0 Msemaji wa timu, jina lake limegeuzwa kinywaji, eti badala ya kuagizwa soda ya 7up, mnunuzi, anasema, nipatie 'Masau Bwire ya baridiiiiii' akimaanisha soda hiyo ya 7up, jamani!


Tuwahakikishie, mashabiki wa Ruvu Shooting, timu ni bora, itafanya tu vizuri katika ligi ya NBC inayoendelea, tuendelee kushikamana na kuiombea mema izidi kufanya vizuri.


Mwisho, niwasihi Watanzania wazalendo, tuendelee kuwa wazalendo, tuipe ushirikiano, tuiombee sana Simba SC, katika mashindano ya kombe la Shirikisho Afrika, ifanye vizuri, ifike hatua ya juu kabisa ya mashindano hayo, itatuheshimisha sana katika ubora wa soka Duniani"


Comments

Popular posts from this blog

Shafii Dauda Nipo Huru Sijafungiwa Na TFF

Gsm Uso Kwa Uso Na Bernard Morrison

Chelsea Bango kubwa linasomeka kutoka Forbes